Jazz yawaleta watu pamoja kuendeleza amani, uhuru na ushirikiano

1 Mei 2013

Siku ya kimataifa ya Jazz imesherehekewa katika nchi 196 kote duniani hapo jana, Aprili 30. Na katika ukumbi wa shule ya upili ya Galatasaray, mjini Istanbul, Uturuki, wasanii maarufu kutoka kote duniani walikutana katika tamasha rasmi la kuadhimisha siku hiyo, na kuendeleza ujumbe wa amani, uhuru na ushirikiano.

Miongoni mwao, alikuwa ni balozi mwema wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Herbie Hancock.

 (SAUTI YA HANCOCK)

“Tangu kuanza kwake Jazz imekuwa kiashiria na kielelezo cha uhuru na demokrasia. Jazz imekuwa sanaa yenye umbo la kimataifa. Muziki wa Jazz unatukumbusha kila siku jinsi tunavyofanana, na kwamba licha ya tofauti za tutokako, sote tuna uwezo wa kuvumiliana. Kupitia kwa jazz, mipaka huvunjwa.”

 Pia miongoni mwa waliohudhuria tamashahilo, ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova

 (SAUTI YA BOKOVA)

 "Jazz huunganisha watu. Jazz huonesha utajiri unaotokana na tofauti zetu. Nguvu za muziki huu zinatokana na utajiri wa mseto wa watu na tamaduni. Jazz ulikuwa mdundo wa karne ya ihsirini, kwa ajili ya mapambano ya utu na haki za watu. Bado ina msukumo katika karne ya ishirini. Jazz inatoa umbo kwa matumaini yetu ya utu, heshima na uhuru. Hii ndio maana UNESCO ilibuni siku ya kimataifa ya Jazz.”

Miongoni mwa wasanii wa Jazz waliotumbuiza ni  Herbie Hancock and Wayne Shorter, Robert Glasper, Esperanza Spalding, Joss Stone, Marcus Miller,  Ramsey Lewis, Hugh Masekela, Keiko Matsui, na wengineo.

 Mwishoni mwa hafla hiyo, mtunzi na msanii maarufu, Wayne Shorter, alitunukiwa medali ya UNESCO ya utamaduni mseto. Siku ya Kimataifa ya Jazz ilianzishwa mwaka 2012, kwa tamasha katika makao makuu ya UNESCO mjiniParis, New Orleans Marekani na katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.