Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNSMIL yafuatilia mwenendo wa maandamano ya wananchi Libya

UNSMIL yafuatilia mwenendo wa maandamano ya wananchi Libya

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Libya UNSMIL unafuatilia kwa karibu hali ya sintofahamu inayoendelea nchini humo ambapo katika siku za hivi karibuni kumekuwa na maandamno mjini Tripoli, kuzunguka majengo ya wizara na taasisi nyingine za serikali.

Akiongea na waandishi wa habari mjini New York msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirsky amesema japo hawezi kueleza kwa undani juu ya hali ya usalama nchini humo kwa sasa, UNSMIL unatambua haki ya Walibya kueleza mahitaji yao kwa njia ya amani lakini pia unasisitiza haja kwa pande zote kuzingatia kanuni na malengo ya mapinduzi ya Libya.

Ujumbe huo umesisitiza kwamba kanuni hizo zinahusu ujenzi wa taifa la sasa na la nguvu kwa misingi ya demokrasia na utawala wa kisheria na haki za binadamu.

UNSMIL umeitaka Walibya kuambatana na kujenga majadiliano ili kutatua tofauti zao kwa kuzingatia kanuni za demokrasia kama njia za kufanikisha malengo ya mapinduzi.