Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo nchini Syria wasababisha mkurupuko wa ugonjwa wa surua

Mzozo nchini Syria wasababisha mkurupuko wa ugonjwa wa surua

Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, limesema mzozo unaoendelea nchini Syria umeharibu vibaya mfumo wa afya, ikiwemo programu ya kitaifa ya utoaji chanjo. Joshua Mmali anayo zaidi kuhusu hali ya Syria

(TAARIFA YA JOSHUA)

Zoezi kubwa la utoaji chanjo linaendelea kwenye nchi walioko wakimbizi wa Syria kwa lengo la kuzuia mkurupko ya ugonjwa wa surua kwa mujibu wa Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF.

Kumeripotiwa mikurupuko kadhaa ya ugonjwa wa surua nchini Syria, Jordan , Lebanon , Iraq na Uturuki.

UNICEF inasema kuwa huku idadi kubwa ya watu wakiendela kuhama na kuzorota kwa huduma za afya nchini Syria tahadhari zinahitaji kuchukuliwa kuhakikisha kuwa watoto wamekingwa dhidi ya ugonjwa wa surua.

Zaidi ya wakimbizi milioni 1.4 wamekimbilia nchi jirani. Ndani mwa Syria watu milioni 4.5 wamalazimika kuhama makwao wengi wakiwa wanaishi kwenye mazingira machafu na magumu. Marixie Mercado kutoka UNICEF anaeleza zaidi.

(SAUTI YA MARIXIE MERCADO)

“Hofu ni dhahiri mno. Hali hii ni ile inayowezesha uenezaji wa magonjwa, na mambo si mazuri kwa raia wa Syria, iwe ndani au nje ya nchi. Hadi sasa hamna watoto walokufa kutokana na surua. Tathmini inaonesha kuwa mikurupuko hii imeweza kudhibitiwa nchini Syria na kwenye ukanda mzima, hasa kwa sababu ya kampeni ya utoaji chanjo mwaka uliopita ilowafikia watu milioni 1.3 na chanjo dhidi ya surua, na watoto milioni 1.5 na chanjo dhidi ya polio.

Wakati UNICEF ikisema hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya mkutano kuhusu hali Mashariki ya Kati, ambapo pia linazingatia barua iloandikwa na ufalme wa Jordan, ukielezea hali ya hatari kwa usalama wake na ule wa kimataifa, kutokana na maelfu ya wakimbizi wa Syria kumiminika nchini Jordan.