UNHCR yaonya dhidi ya kuwalazimisha wakimbizi wa CAR kurudi makwao katika mazingira ya ghasia

UNHCR yaonya dhidi ya kuwalazimisha wakimbizi wa CAR kurudi makwao katika mazingira ya ghasia

Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi, UNHCR, limesema kwamba wakimbizi waliokimbia mapigano Jamhuri ya Afrika ya Kati hawapaswi kulazimishwa kurudi nyumbani. Joseph Msami na taarifa zaidi.

(SAUTI YA MSAMI)

 Shirika hilo linasema bado hali ya usalama nchini humo ni tete, huku kukiwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kuzorota kwa hali ya kibinadamu.

Hali imekuwa hivyo tangu mwezi Disemba mwaka jana pale waasi wa Seleka walipoanzisha mashambulizi kaskazini mwa nchi na badaye kuuteka mji mkuu Bangui mwishoni mwa mwezi Machi.

Makadirio ya awali yanaonyesha kuwa idadi ya watu waliopoteza makazi ndani ya nchiyao kutokana na ghasia hizo  ni zaidi ya laki na sabini huku takribani watu Elfu Hamsini wakiwa wamekimbilia nchi jirani za Jamhuri ya kidemokrasia yaKongo, Chad na Cameroon.

 Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR.

 (SAUTI YA ADRIAN EDWARD)

Kwa mazingira ya sasa, watu wengi wanaokimbia mapigano Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaweza kukidhi mkataba wa uliokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika na mkataba wa mwaka 1951 kuhusu vigezo vya  hadhi za wakimbizi . Wakati hayo yakijiri, mauaji ya kudhamiria, ukamataji wa holela, na kuwekwa vizuizini, mateso, pamoja na ajira ya watoto vimeripotiwa kwa ukubwa. Ubakaji, kupotea,  utekaji nyara, ulafi na uporaji mjini Bangui na sehemu nyingine za mji pia vimeripotiwa. Ufikiwaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu walioathirika bado unakumbwa na vikwazo. Lengo letu katika kutoa ushauri huu ni kuona kanuni za kibinadamu na hifadhi zinazingatiwa hadi pale hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati inaruhusu urejeaji ulio na hadhi na wa kiusalama.”