Mkutano wa kwanza wa ILO wafanyika Myanmar tangu kupitishwa sheria ya uhuru wa kukusanyika

30 Aprili 2013

Mwaka mmoja baada ya serikali ya Myanmar kupitisha sheria za masuala ya kazi wajumbe kutoka mashirika 500 ya kazi wamekusanyika kwenye mkutano wa maalumu kujadili masuala ya ujuzi kazini , maamuzi ya pamoja na afya na usalama kazini miongono mwa ajenda nyingi zilizoandaliwa ambazo ni muhimu kwa wafanyakazi nchini humo.

Naibu mkurugenzi wa ILO katika masuala ya utumishi na mabadiliko kazini Greg Vines wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili mjini Yangon amewaambia washiriki wa mkutano kwamba mkutano huo ni taswira nzuri ya uhuru wa kukusanyika ambao ulianzishwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita unaojumuisha haki ya mikutano na kuongea katika kuijenga upya Myanmar.

Naye naibu waziri wa kazi wa Myanmar U Myint Thein amewaambia washiriki wa mkutano kwamba mabadiliko na mashirika hayo mapya ya kazi yaliyoanzishwa yatakuwa tofauti nay a zamani na yatakuwa na uhuru wa kujiwekea ajenda zake, na kuongeza kuwa serikali inajitahidi kukomesha mifumo yote ya ukandamizaji kazini, ili kutoa fursa za kazi kwa vijana, na makundi mengi yaliyosahaulika.

ILO imeanzisha miradi ya uhuru wa kukusanyika kusaidia nchi kutekeleza sheria za kazi za kimataifa zilizopitishwa na shirika hilo. Mradi huo unafadhiliwa na Marekani na unatoa elimu na mafunzo kwa wafanyakazi, wamiliki wa biashara na maafisa wa serikali.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud