Baraza la usalama lasikitishwa na hali ya usalama Jamhuri ya Afrika ya Kati

29 Aprili 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeeleza wasiwasi wake mkubwa juu ya kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama huko Jamhuri ya Afrika ya Kati na kutaka mamlaka husika zirejeshe amani, utulivu na usalama kwenye mji mkuu Bangui.

Tamko hilo ni kwa mujibu wa taarifa ya Baraza hilo iliyotolewa mwishoni mwa kikao cha mashauriano kuhusu nchi hiyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa mkuu wa masuala ya kisiasa ndani ya Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman.

Wajumbe wa Baraza wametaka pande husika kuwezesha makundi yanayotoa misaada ya kibinadamu kuwafikia walengwa na kwamba viongozi wa kundi la Seleka wahakikishe wafuasi wao wenye silaha wanajiepusha na vitendo vya ghasia na kurejea kwenye kambi zao kwa mujibu wa makubaliano ya Libreville.

Pamoja na kupongeza utendaji kazi wa watumishi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa BINUCA, pia wameelezea utayari wao wa kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua zaidi za kuleta utulivu nchini humo.

Baraza la Usalama limetia matumaini katika mkutano wa tarehe Tatu mwezi ujao utakaofanyika Brazaville, pamoja na juhudi za taasisi za kikanda ukiwemo Umoja wa Afrika na kumtaka Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kutumia madaraka yake kwa mujibu wa makubaliano ya Libreville na N’Djamena ili kuweka utulivu.