Skip to main content

Ban amteua Modibo Toure kuwa Mshauri Maalum wa mjumbe wake wa Maziwa Makuu

Ban amteua Modibo Toure kuwa Mshauri Maalum wa mjumbe wake wa Maziwa Makuu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, leo amemteua Bwana Modibo Toure kama Mshauri Maalum wa Mjumbe wake katika ukanda wa Maziwa Makuu, Mary Robinson.Tangu mwezi Januari mwaka huu, Bwana Toure ambaye ni raia wa Mali, amekuwa akihudumu kama mratibu mkaazi wa masuala ya kibinadamu na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa mjini Nairobi, Kenya.

Wajibu wake utahusisha kumsaidia Bi Robinson katika juhudi za kutekeleza mkakati wa amani na usalama na ushirikiano kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambao ulisainiwa na nchi 11 za ukanda wa Maziwa Makuu mnamo Februari 24 mjini Addis Ababa.

Bi Robinson yupo sasa ziarani katika ukanda wa Maziwa Makuu tokea leo Aprili 29 hadi tarehe 5 Mai. Ziara hiyo inampeleka Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Uganda, Burundi na Addis Ababa kwenye makao makuu ya Muungano wa Afrika.