Huduma za posta kurejea Somalia, baada ya kukosekana kwa miaka 23

29 Aprili 2013

Somalia imetiliana saini na falme za kiarabu makubaliano ya kusaidia urejeshaji wa huduma za posta nchini humo baada ya kukosekana kwa miaka 23 kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.Makubaliano yalitiwa saini kwenye makao makuu ya UPU nchini Uswisi na ambapo kwa mujibu wa makubaliano hayo, mji wa Dubai utakuwa kitovu cha kupokea barua zote za kigeni za Somalia na hatimaye zitasafarishwa kwa ndege zinazokwenda mji mkuu Mogadishu.

Mkurugenzi Mkuu wa UPU Bishar Hussein amesema huo ni mwanzo na kwamba taratibu zote zikikamilika miezi michache ijayo, shirika lake litajulisha wanachama 192 juu ya kuanza kwa huduma za posta nchini Somalia.

Naye Waziri wa Somalia wa masuala ya posta, Abdullahi Hersi amesema wakati umefika kwa serikali kuanza kutoa huduma za posta kwani mawasiliano ni haki ya binadamu na kwamba watu wanaweza kuwa na huduma za intaneti na simu lakini hizo haziwezi kuziba pengo la faida za kupokea barua au kifurushi kutoka mbali.

Mwaka 1991 Somalia ilikuwa na ofisi 100 za posta na watumishi zaidi ya Elfu Mbili lakini hii leo kuna ofisi kuu moja ya posta kwenye mji mkuu Mogadishu ikiwa na wafanyakazi 25.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter