Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya Iraq inatisha, hatua za haraka zichukuliwe - Kobler

Hali ya Iraq inatisha, hatua za haraka zichukuliwe - Kobler

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Martin Kobler, ametaka pande zote nchini Iraq kujizuia na mapigano na badala yake kuwepo kwa mjadala mkuu nchini humo kufuatia mapigano ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo na majeruhi kwa mamia ya watu nchini humo.

Bwana Kobler ameelezea hofu yake juu ya nchi kuelekea kusikojulikana ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa kukomesha ghasia zinazojirudia mara kwa mara nchini Iraq.

Amewataka viongozi wa dini na siasa nchini Iraq kutoiacha hasira ishinde dhidi ya amani na kutumia busara zao katika kurejesha amani. Amesema ni jukumu la viongozi wote wa nchi kuchukua hatua za kijasiri kama vile kukaa pamoja na kutaka kwa pamoja urejeshwaji wa haraka wa utulivu na mjadala wa kitaifa kwa mapana.

Pia Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq amewataka viongozi wa serikali kuendesha uchunguzi wa uhakika na wa wazi kuhusu matukio katika eneo la Hawija ambapo mapigano yaliibuka kati ya waandamanaji na vikosi vya ulinzi na kurejelea wito wake wa kuachiliwa kwa wafungwa waliokamatwa wakati wa msako.