Umoja wa Mataifa wakaribia kupeleka ujumbe wa UNAMSOM Somalia

25 Aprili 2013

Umoja wa Mataifa unaendelea kufanya kazi na serikali ya Somalia na mamlaka za mikoa ili kuweka ujumbe mpya wa Umoja wa Mataifa wa kuisaidia Somalia, UNAMSOM, kwa ajili ya kuendeleza amani na kulijena tena taifa hilo, kama lilivyoazimia Baraza la Usalama katika azimio namba 2093 (2013).

Akilihutubia Baraza la Usalama hii leo, Mkuu wa Masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Mataifa, Jeffrey Feltman amesema hivi sasa inafahamika dhahiri jinsi Umoja wa Mataifa unavyotakiwa kuisaidia serikali ya Somalia hadi mwaka 2016.

(SAUTI YA FELTMAN)

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, amesema kuongeza uwezo wa Wasomali wa kudhibiti mambo na kuusaidia uongozi wake utakuwa sehemu muhimu ya juhudi za Umoja wa Mataifa za kuimarisha harakati za amani.

Aidha, ameongeza kuwa katika siku zijazo, anatumai kuwa ni masuluhu yanayobuniwa na Wasomali wenyewe ndiyo yatakayosaidia kumaliza mizozo na kutoa mwongozo bora wa kuiendeleza Somalia.