Mtaalamu wa haki za binadamu wa UM kukusanya taarifa za wakimbizi wa Eritrea

25 Aprili 2013

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Eritrea Sheila B. Keetharuth, atafanya ziara ya kikazi Ethiopia na Djibouti kuanzia tarehe 30 Aprili hadi 9 May 2013 ili kukusanya moja kwa moja taarifa kutoka kwa wakimbizi wa Eritrea kuhusu hali ya haki za binadamu nchini mwao.

Amesema kutokana na kutokuwa na uwezekano wa fursa ya kuzuru Eritrea atashirikiana na wote ambao wanahofia hali ya haki za binadamu Eritrea ikiwa ni pamoja na wanaojichukulia kama wahanga wa ukiukahji wa haki za binadamu , watetezi wa haki za binadamu na wadau wa jumuiya za kijamii.

Katika ziara yake hii ya kwanza kwa wakimbizi atakusanya taarifa kutoka kwa wakimbizi wenyewe wa Eritrea ambao wamekimbilia nchi jirani za Ethiopia na Djibout ambako serilikali zimekubali kumruhusu kutembelea wakimbizi hao.

Tangu alipoteuliwa Novemba 2012 mwakilishi huyo ameomba mara kadhaa kuzuru Eritrea lakini hadi sasa hajapatiwa fursa hiyo.

Amerejea kuitaka serikali ya Eritrea kushirikina na uongozi wake kwa lengo la kushughulikia suala la changamoto za haki za binadamu.

Akiwa ziarani atawahoji wakimbizi wa Eritrea walioko makambini ili kutathimini madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu aliyoyapata kutoka vyanzo mbalimbali.

Na matokeo ya tathimini yake yatatolewa kwenye ripoti yake ya kwanza kwa baraza la haki za binadamu mwezi Juni mwaka huu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud