Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyandarua ni muhimu katika kupunguza vifo vitokanavyo na Malaria: UNICEF

Vyandarua ni muhimu katika kupunguza vifo vitokanavyo na Malaria: UNICEF

Ugonjwa wa Malaria unaua watu Laki Sita na sitini kila mwaka na wengi wao ni watoto barani Afrika, lakini iwapo kila mtu duniani ataweza kutumia vyandarua vyenye viuatilifu tunaweza kuishinda Malaria. Huo ni ujumbe wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF hii leo katika kuadhimisha siku ya Malaria duniani.  UNICEF na washirika wake inatia shime na kusadia serikali kusambaza bure kwa wananchi wao vyandarua hivyo ambapo imesema matumizi ya chandarua kimoja kwa watu wawili yanaweza kupunguza vifo vya watoto kwa karibu asilimia 20.  Mkurugenzi wa programu za UNICEF Nicholas Alipui anasema ni jambo lisilokubalika kuwa kila siku zaidi ya watoto Elfu Moja Mia Tano wanakufa kutokana na ugonjwa wa Malaria ambao unatibika na pia una kinga. Lakini amesema bado ugonjwa huo ni tishio barani Afrika kwa kuwa watoto wengi hawalali ndani ya vyandarua. UNICEF inasema awali tatizo lilikuwa ni upatikanaji wa vyandarua hivyo ambapo mwaka 2004 kulikuwa na vyandarua Milioni Tano na Laki Sita katika nchi za AFrika zilizo kusini kwa jangwa la Saharal akini hivi sasa kutokana na uwekezaji mzuri kwenye sekta ya kuzalisha vifaa hivyo kuna vyandarua Milioni 145.