Siku ya Malaria duniani, bado Afrika yazidiwa mzigo: Ban

25 Aprili 2013

Katika kuadhimisha siku ya Malaria duniani hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa ujumbe na kusema kuwa bado ugonjwa huo ni mzigo kwa nchi maskini hususan barani Afrika ambako mamilioni ya watu wanashindwa kujikinga dhidi ya Malaria.  Bwana Ban amesema barani Afrika kila dakika mtoto mmoja anafariki dunia kutokana na ugonjwa huo na kwamba mifumo dhaifu ya ufuatiliaji inakwamisha uwezo wa serikali na shirika la afya duniani, WHO kupata taarifa za kina kuhusu maeneo mapya yenye ugonjwa huo na mabadiliko ya mwenendo wa ugonjwa huo. Amesema usugu wa vijidudu vya Malaria dhidi ya dawa za kunywa na hata katika vyandarua vyenye viuatilifu, unafanya hali kuwa mbaya zaidi kuweza kutokomeza ugonjwa huo na hivyo kutishia uhai na maendeleo.

Bwana Ban amesema katika siku ya leo yenye ujumbe wekeza kwa baadaye, tokomeza malaria, ameisihi jumuiya ya kimataifa ikiwemo wanasiasa katika nchi zinazotishiwa na ugonjwa huo kuwekeza fedha na kuendeleza azmayaoya kuhakikisha kila mwananchi anaweza kujikinga dhidi ya Malaria.