Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suala la Mashariki ya Kati lamulikwa tena na Baraza la Usalama

Suala la Mashariki ya Kati lamulikwa tena na Baraza la Usalama

Mizozo na harakati za amani Mashariki ya Kati vimemulikwa tena na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wiki moja baada ya Baraza hilo kuelezwa kwa kina kuhusu baa linaloibuka nchini Syria, wakati mgogoro unapoendelea kutokota. Grace Kaneiya na taarifa kamili(TAARIFA YA KANEIYA)

Kikao cha leo cha Baraza la Usalama pia kimehudhuriwa na kuhutubiwa na wawakilishi wa Israeli na Palestina.

Akiongea katika mkutano huo, Mkuu wa Masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Mataifa, Jeffrey Feltman, amesema, wakati hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota kutokana na mzozo wa Syria unao-onekana kutopata suluhu la kisiasa, suala la mzozo wa Israeli na Palestina linatakiwa pia kuzingatiwa.

Ni wakati wa hatari zaidi na ukosefu wa usalama kote Mashariki ya Kati. Kuna haja ya kuchukua hatua haraka kukabiliana na masuala ya kibinadamu ndani na nje ya Syria.

Lebanon na Jordan zinapaswa pia kusaidiwa kikamilifu. Hatua inatakiwa pia kuchukuliwa kuhusu suala la Israel na Palestina.

Matumaini machache yaliyofufuliwa tena na uingiliaji kati wa Marekani, yanatakiwa kuendelezwa na kufanywa kuwa juhudi za dhati za pande husika.

Bwana Feltman amesema hamu ya kuwa na amani inatakiwa iwekwe kwa kuchukuwa hatua za mapema kumaliza uhasama na kujenga imani.

Bwana Feltman ameliambia Baraza la Usalama kuwa hali ya kiuchumi Palestina ni mbaya mno, inahitaji msaada zaidi kutoka jamii ya kimataifa.

Amesema pia hali ya kibinadamu ya wafungwa wa Kipalestina pia inatia wasiwasi, na inahataji kuzingatiwa, kwani imechangia sana machafuko katika ukanda huo.