Leo ni siku ya kimataifa ya vitabu na hati miliki:UNESCO

23 Aprili 2013

Leo ni siku ya Kimataifa ya vitabu na hati miliki . Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO limekuwa likiadhimisha siku hii kila tarehe 23 April kwa miaka 17 sasa.Nchi wanachama wa UNESCO wanaadhimisha siku hii kwa kutambua umuhimu na uwezo wa vitabu kuwaleta watu pamoja na kuelimisha kuhusu utamaduni wa watu na ndoto zao za mustakhbali bora hapo baadaye.

Katika ujumbe wake maalumu kuhusu siku hii mkurugenzi mkuu wa UNESCO Irina Bokova amesema siku mhii inatoa fursa ya kutafakari kwa pamoja njia nzuri za za kuelimisha kuhusu utamaduni ulioandikwa vitabuni na kuruhusu watu wote wanaume , wanawake na watoto kupata ujumbe huo kupitia programu maalumu ya kufuta ujinga na kuunga mkono fani ya uchapishaji vitabu , maduka ya uuzaji vitabu, maktaba mbalimbali na pia mashuleni.

Ameongeza kuwa vitabu ni mshirika mkubwa wa kusambaza elimu, sayansi, utamaduni na taarifa duniani kote.

Mwaka huu mji wa Bankok Thailand ndio ulioteuliwa kuwa “Mji mkuu wa vitabu mwaka 2013” kwa kutambua programu zake za kuchagiza usomaji vitabu miongoni mwa vijana na watu wasio na uwezi katika jamii.

Siku hii ni mahsusi kwa ajili ya kuchagiza elimu na usomaji , lakini pia kulinda hati miliki ya upatikanaji na utajiri wa vitabu duniani.