Utoaji wa silaha kwa pande zinazozozana Syria ukomeshwe: Ban

22 Aprili 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Matiafa, Ban Ki-moon, amesema utoaji wa silaha kwa pande zinazozozana nchini Syria wafaa ukomeshwe, akiongeza kuwa silaha zaidi zinamaanisha vifo zaidi, na uharibifu zaidi.

Bwana Ban amesema hayo katika taarifa ilotolewa mara tu baada ya mkutano wake na Sheikh Hamad bin Jassim bin Jabr Al-Thani, Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa la Qatar, na Bwana Nabil Elaraby, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Akielezea kusikitishwa na hali inayoendelea kuzorota nchini Syria ambako thuluthi moja ya idadi nzima ya watu wanahitaji msaada wa dharura, Bwana Ban amerejelea wito wake kwa nchi wafadhili kuunga mkono kikamilifu juhudi za Umoja wa Mataifa za kutoa huduma za kibinadamu.

Katibu Mkuu pia amesisitiza kuwa hapawezi kuwepo suluhu lingine la kuumaliza mgogoro wa Syria, ila suluhu la kisiasa, na kusema hiyo ndiyo maana ya kuhitajika haraka mazungumzo kati ya pande zinazozozana.

Akizungumza kuhusu harakati za amani Mashariki ya Kati, Bwana Ban amesema anaendelea kuwasihi Waisraeli na Wapalestina kuongeza juhudi za kufikia makubaliano wa masuala yote muhimu yanayouhusu mzozo kati yao, hasa mwaka huu 2013, akiongeza kuwa fursa iliyopo sasa hivi isipotezwe.