Ban ashtushwa na ghasia na mauaji Borno Nigeria:

22 Aprili 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameshtushwa na kushangazwa na ripoti za idadi kubwa ya vifo vya raia na uharibifu wa nyumba uliosababishwa na mapigano baina ya majeshi na makundi yenye itikadi kali kwenye mji wa Kaskazini wa Baga jimbo la Borno nchini Nigeria.

Machafuko hayo yalitokea April 19 na Aprili 20 mwaka huu, na Ban ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizoathirika na kupoteza ndugu na jamaa zao huku akitoa wito kwa makundi yote yenye msimamo mkali kusitisha mashambulizi.

Katibu Mkuu amerejea msimamo wake kwamba hakuna kitu au sababu yoyote inayohalalisha ukatili huo au matumizi ya ghasia. Amezitaka pande zote husika Nigeria kuzingatia na kuheshimu sheria za kimataifa na kulinda haki za binadamu.