Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu alinde sayari dunia kwa mustakhbali wa wote: UM

Kila mtu alinde sayari dunia kwa mustakhbali wa wote: UM

Wakati mustkhbali wa dunia uko hatarini kutokana na vitendo vinavyohatarisha uwepo wa sayari hii, kila mkazi ametakiwa kuwa makini katika kuhifadhi na kulinda mazingira kwa kuwa hakuna pahala pengine pa kukimbilia na huo ni wito kwa siku ya kimataifa ya kulinda sayari dunia hii leo kama anavyoripoti Grace Kaneiya. (PCKG- Grace)

Kauli hizo zimetolewa mjini New York, Marekani, wakati wa mazungumzo ndani ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha siku ya sayari dunia. Rais wa Baraza Kuu Vuk Jeremic amesema ustawi wa dunia unategemea kuishi sambamba na mazingira asili badala ya binadamu kufanya shughuli zinazoharibu mazingira.

(SAUTI YA VUK)

“Kwa sasa limekuwa ni jambo linalokubalika sana kama mwenendo wa sera ya umma kwamba maendeleo na hatma ya binadamu yanafaa kwenda pamoja na mtazamo wa maendeleo endelevu.”

Naye katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema siku hii ni fursa muhimu kwa kila mtu kurejelea wajibu wa pamoja wa kuishi bila kuharibu mazingira wakati huu ambapo sayari hii inakabiliwa na vitisho mbali mbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi.

(SAUTI YA BAN)

“Hivi sasa tunapaswa kukabiliana na ukweli unaouma ya kwamba sayari yetu iko hatarini, mabadiliko ya tabianchi ni bayana na tatizo linalokua.”