UNICEF yalaani kubakwa kwa mtoto wa miaka mitano India

22 Aprili 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limelaani kitendo cha kubakwa kwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitano hukoNew Delhi,India. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

(Taarifa Assumpta)

Katika taarifa yake, UNICEF imesema kitendo dhidi ya mtoto huyo ni dalili dhahiri kuwa hatua za pamoja na za dharura zahitajika ili kuhakikisha wasichana na wanawake nchini humo wanaweza kujisikia wako salama wakiwa wanatembea njiani, wakiwa shuleni na hata wakiwa kazini na majumbani.

UNICEF imeeleza kuguswa na kitendo hicho na kumtakia mtoto huyo ahueni ya haraka.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa zaidi ya vitendo Elfu 30 vya uhalifu vilifanywa dhidi ya watoto nchini India mwaka 2011 na kwamba mhanga mmoja kati ya watatu wa vitendo vya ubakaji ni mtoto.

Tukio hilo linakuja miezi mitano tangu msichana abakwe hadi kufa nchini humo.