Nishati endelevu ni muhimu kwa maendeleo:Ban

19 Aprili 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema nishati endelevu ni muhimu kwa karibu kila changamoto zinazokabili dunia ikiwamo kuwakwamua watu kutoka kwenye umaskini kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabia nchi, kuwezesha biashara, shule na kuboresah huduma za kliniki ili kuwawezesha wanawake.

Akifungua mkutano wa bodi ya ushauri wa nishati endelevu mjiniWashington, Bwana Ban amesema nishati ni dhana muhimu katika mijadala ya mkakati wa maendeleo baada ya 2015 na kusisitiza uhakika wa faida za nishati ya kisasa kuwafikia wote.

Katibu huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ametaka ushirikiano kati ya serikali, asasi za kiraia na biashara akianisha jukumu muhimu la asasi hizo katika kuwafikia wahitaji ili kutimiza malengo na vipaumbele.

(SAUTI YA BAN)

"Tumeweka malengo na vipaumbele vitatu, kutoa huduma ya umeme na nishati kwa watu wote duniani, pili inabidi tuongeze ufanisi wa nishati na tatu ni kuongeza nishati mbadala. Kutimiza malengo haya itawezeha usawa wa kijamii, kusaidia kuimarisha uchumi wa dunia na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Nishati endelevu kwa wote ni alama ya ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Benki ya dunia."