Siku ya kimatiafa ya kuilinda dunia kuadhimishwa tarehe 22 mwezi huu

18 Aprili 2013

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO liko kwenye mstari wa mbele katika maandalizi ya siku ya kimataifa ya kuilinda dunia ambayo itaadhimishwa tarehe 22 mwezi huu.Balozi mwema wa FAO Khaled ambaye ni mwanamuziki maarufu kutoka Algeria, atatumbuiza siku hiyo akishirikina na mwanamuziki kutoka Italia Fiorella Mannoia mjini Milan.

Jumatatu ijayo zaidi ya watu bilioni moja kote duniani watashiriki kwenye maadhimisho ya 43 ya siku ya kimataifa ya kuilinda dunia.

Kauli mbiu ya mwaka huu itakuwa sura ya mabadiliko ya hali ya hewa. Siku hii inatarajiwa kutoa hamasisho kuhusu athari za mabadiliko ya hali ya hewa kama vile ukame wa muda mrefu, mafuriko ya mara kwa mara, vimbunga, kupanda kwa maji ya bahari na kadhalika.

Rais wa siku hiyo Pierluigi Sassi anasema kuwa sherehe hizo zitazindua kampeni ya miaka mitatu hadi mwaka 2015 ambayo itaangazia umuhimu wa ulimwengu wenye afya kwa misingi kuwa ulimwemgu wenye afya ni kiungo muhimu cha kuwepo chakula cha kutosha.