Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usimamizi wa Haki za binadamu katika sekta ya biashara Marekani kumulikwa

Usimamizi wa Haki za binadamu katika sekta ya biashara Marekani kumulikwa

Jopo la wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na haki za binadamu litakuwa na ziara ya siku 10 nchini Marekani, lengo ni kuangalia iwapo sekta ya biashara nchini humo inazingatia mwongozo wa biashara na haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Mmoja wa wataalamu hao Michael Addo amesema ziara hiyo ni mwaliko wa serikali, na itaaanza tarehe 22 mwezi huu ambapo watatembelea maeneo kadhaa ikiwemo Arizona, California na Florida na watazungumza na wamiliki, wafanyakazi na wadau wengine.

Amesema Marekani imejumuisha ajenda ya haki za binadamu katika sekta ya biashara kwa hiyo wanataka kujifunza jitihada za serikali za kutekeleza mwongozo huo uliopitishwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwaka 2011.

Mwongozo huo unatoa maelekezo bayana ya jinsi mamlaka na kampuni zinaweze kutimiza wajibu wao bila kukiuka haki za binadamu na kuchukua hatua mara moja iwapo tatizo linajitokeza.

Ripoti ya ziara hiyo itawasilishwa kwenye kikao cha baraza la haki za binadamu mwezi Julai mwakani.