Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mawaziri wa Fedha wakutana Washington, Marekani

Mawaziri wa Fedha wakutana Washington, Marekani

Mawaziri wa fedha na viongozi wengine kutoka kote duniani wanakutana mjini Washington, DC Marekani katika mkutano wa kila mwaka unaoandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, IMF.

Miongoni mwa wale wanaohudhuria mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye amesema anataraji mkusanyiko huo wa viongozi wa ngazi ya juu utageuzwa kuwa uungaji mkono wa ngazi ya juu wa malengo ya maendeleo ya milenia.

Kabla ya mkutano huo, Bwana Ban amesema mambo manne muhimu yataangaziwa.

 (SAUTI YA BAN)

"Kwanza, ni elimu. Hii ni moja ya uwekezaji wenye busara zaidi tunaoweza kufanya kwa ajili ya siku zijazo. Pili, mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo endelevu, na nishati endelevu. Tatu, umaskini- tumepiga hatua kubwa, lakini bado kuna kazi nyingi ya kufanya, na ni lazima tuchukue hatua katika kipindi hiki. Nne, mchango wa benki za maendeleo."

Wakati wa mkutano huo, rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, Katibu Mkuu Ban Ki-moon na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Gordon Brown, wataongoza kikao cha mawaziri kuhusu Elimu kwa Wote, ili kujadili hatua zinazoweza kuchukuliwa na serikali na wadau ili kuwapeleka watoto wote shule na kuboresha matokeo ya elimu.