Mamilioni ya watoto duniani wakosa chanjo muhimu: WHO

17 Aprili 2013

Ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa maadhimisho ya wiki ya utoaji chanjo duniani tarehe 20 mwezi huu, Shirika la afya duniani, WHO limesema takribani watoto Milioni 22 hususan katika nchi zinazoendelea hawajapatiwa chanjo za msingi za kuwakinga dhidi ya magonjwa hatari. WHO inasema mifumo dhaifu ya utoaji wa huduma za afya pamoja na migogoro ni miongoni mwa sababu zinazowanyima watoto haki ya kupata chanjo za kimsingi dhidi ya magonjwakamavile Surua, kifaduro, polio, dondakoo na pepopunda. Shirika hilo linasema ni vyema kuelimisha umma juu ya faida za watoto kupata chanjo na madhara iwapo hawatapatiwa. Mkuu wa kitengo cha chanjo ndani ya WHO Dkt. Jean-Marie Okwo-Bele, anasema chanjo dhidi ya magonwja hayo huepusha vifo vya watoto Milioni Tatu kila  mwaka.

 (Sauti ya Dkt.Jean-Marie)

 “Takribani asilimia 80 ya watoto wachanga duniani kote wamepata chanjo za msingi na hiki ni kiwango cha juu ukilinganisha na mipango mingine ya afya ya umma. Lakini bado kuna pengo la asilimia 20 la kufikia watoto wote duniani, na kiwango hicho ni kikubwa na hii ina maana bado tuko nyuma katika kufikia mathalani lengo la kutokomeza polio. Tunashuhudia wahudumu wa afya wakiuawa kwa sababu wanatoa huduma za kulinda uhai. Sote tunaapswa kuwa thabiti kushutumu na kutaka vitendo hivyo vikomeshwe.”

Aidha Dkt. Okwo-Bele amesema fikra potofu zisizo na msingi ya kwamba chanjo hazina ufanisi wowote zimesababisha kuibuka kwa magonjwa kama vile Surua katika nchi zilizoendeleakamavile Ufaransa, Hispania na Uingereza.