Umaskini umepungua duniani lakini bado kuna changamoto kubwa: Benki ya Dunia

17 Aprili 2013

Ripoti ya Benki ya Dunia imesema kuwa idadi ya watu wanaoishi kwa chini ya dola moja na robo kila siku imepungua kwa kiwango kikubwa katika miongo mitatu iliyopita kutoka nusu ya idadi nzima ya watu duniani mwaka 1981, hadi asilimia 21 tu mwaka 2010, licha ya idadi ya watu maskini kupanda kwa asilimia 59 katika nchi zinazoendelea.

Hata hivyo, tathmini mpya ilotolewa na Benki ya Dunia inaonesha kuwa bado kuna watu bilioni 1.2 ambao bado wanaishi katika umaskini wa kupindukia, na licha ya kupiga hatua kubwa hivi karibuni, eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara bado linachangia zaidi ya theluthi moja ya watu maskini zaidi duniani.

Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, amesema idadi ya watu ambao bado wanaishi katika umaskini ulokithiri inatakiwa ichukuliwe kama mbiu ya mgambo kwa jamii ya kimataifa kuongeza kasi ya kupiga vita umaskini. Amesema kwa ushauri na tathmini ya Benki ya Dunia, njia inaweza kupatikana ya kuutokomeza umaskini ulokithiri ifikapo mwaka 2030, kwa kuonesha ni wapi umaskini ulipo, na ni wapi ulipokithiri.

Ripoti hiyo imetolewa siku moja kabla ya mkutano wa kila mwaka wa mawaziri wa fedha kutoka kote duniani, ambao umeandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, IMF kuanzia kesho mjini Washington, D.C. Marekani, ambao pia utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.