Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mali, DRC, CAR, na Syria kwenye ajenda ya mkutano wa Ban na waandishi wa habari

Mali, DRC, CAR, na Syria kwenye ajenda ya mkutano wa Ban na waandishi wa habari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amekutana na waandishi wa habari mjini New York na kuzungumza kuhusu masuala mseto yanayohusu amani na usalama.Miongoni mwa nchi alizoangazia katika mkutano huo, ni Mali, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Syria na Jamhuri ya Watu wa Korea Kaskazini, DPRK. Kuhusu Syria, Bwana Ban amesema baa la vita nchini humo linazidi kuzorota kila siku mapigano yanapoendelea.

"Harakati za kijeshi zinaiharibu nchi na kutia ukanda mzima katika hatari. Raia ndio wanaoathirika zaidi, na ni lazima walindwe. Umoja wa Mataifa unafanya uwezalo kutoa huduma za kibinadamu za dharura na kusaidia kwa mzigo wa zaidi ya wakimbizi milioni moja kwa nchi jirani za Syria. Matumaini huenda yasioenekane kwa urahisi, lakini bado naamini kuwa suluhu la kisiasa linawezekana."

Bwana Ban amesema atafanya mazungumzo na mwakilishi maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Nchi za Kiarabu, Lakhdar Brahimi ili kuangazia kinachoweza kufanywa. Ameahidi kufuatilia uchunguzi wa ripoti za matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria.

Kuhusu Mali, Bwana Ban amesema hali ya usalama imeboreka kwa ajili ya uingiliaji kati wa vikosi vya Ufaransa na vikosi vya Kiafrika. Hata hivyo, amesema bado kuna jukumu kubwa la kurejesha uongozi wa kisheria na udhibiti wa mipaka ya Mali, na maendeleo ya kisiasa yatahitajika kwa suluhu la kudumu.

Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bwana Ban amesema ameshangazwa na mapigano nchini humo,

Natoa wito kwa walio mamlakani sasa kurejesha uongozi wa kisheria na utaratibu nchini humo. Nakaribisha juhudi za Muungano wa Afrika na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati, ECAS kuendeleza amani.”

Bwana Ban pia amezungumza kuhusu hatua zilizopigwa katika kutafuta amani katika DRC, kama vile azimio la kuongeza nguvu za kijeshi za MONUSCO na kumteua Bi Mary Robinson kama mwakilishi maalum wa eneo la Maziwa Makuu.

Maeneo mengine aliyozungumzia ni Mashariki ya Kati, na rasi ya Korea. Amesema harakati za amani Mashariki ya Kati bado ni jambo la kipaumbele.

Amesema anakaribisha kukubali kwa DPRK kufanya mazungumzo, na kuitaka DPRK ibadili mkondo wake wa kuunda silaha za nyuklia, huku akiiomba jamii ya kimataifa isipuuze hali ya kibinadamu na haki za binadamu katika DPRK.