Mwandishi aliyeko gerezani ashinda tuzo ya Uhuru wa vyombo vya habari

17 Aprili 2013

Mwanahabari wa Ethiopia anayetumikia kifungo nchini humo Reeyot Alemu ameshinda tuzo la uhuru wa vyombo vya habari duniani la shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO kwa mwaka huu wa 2013, inayoitwa UNESCO Guillermo Cano.

Mwandishi huyo wa habari mwanamke, alipitishwa na jopo huru la majaji wataalamu katika fani hiyo kwa kuzingatia ujasiri wake wa kipekee, ushindani na dhamira katika uhuru wa kujieleza. Pia jopo hilo lilizingatia mchango wa Alemu katika machapisho huru ambapo aliandika kwa kina kuhusu siasa na msuala ya jamii akiangazia katika chanzo cha umaskini na usawa wa kijinsia.

Reeyote ambaye amefanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari binafsi, mwaka 2010 alianzisha chapisho lake lililoitwa Change lililofungiwa mwaka mmoja baadaye na wakati anafanya kazi ya uandishi wa habari katika gazeti liitwalo Feteh, alikamatwa na sasa anatumikia kifungo cha miaka mitano jela .

Tuzo ya UNESCO Guillermo Cano ilianzishwa mwaka 1997 na bodi ya UNESCO ambapo hutolewa kila mwaka wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari tarehe 31 mwezi Mei na mwaka huu yatafanyika Costa Rica.