Baraza la Usalama lamulika ukatili dhidi ya wanawake katika vita

17 Aprili 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya kikao maalum kuangazia suala la ukatili wa kingono dhidi ya wanawake katika mazingira ya vita, kikao ambacho kilianza kwa kutoa heshima kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher na wahanga wa mabomu wakati wa mbio za Boston Marathon. Joshua Mmali na taarifa kamili.

(Taarifa ya Joshua)

Akilihutubia Baraza hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema ni muhimu kuzingatia suala la ukatili wa kingono wakati wa mazungumzo ya amani na makubaliano ya kusitisha mapigano, na kuhakikisha wahalifu wamewajibika kisheria kama njia ya kuzuia ukatili kama huo.

(SAUTI YA BAN)

“Ubakaji wakati wa vita hauharibu tu maisha ya watu binafsi, unaharibu pia familia na jamii nzima. Pia ni kizuizi kwa maridhiano na maendeleo endelevu. Madhara ya ubakaji katika vita hudumu muda mrefu hata baada ya vita kuisha. Ni lazima tuimarishe juhudi zetu za kuzuia ukatili wa kingono, kama suala la kimsingi.”

Naye Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili dhidi ya wanawake katika maeneo ya vita, Zainab Hawa Bangura, amesema waathirika wa ukatili wa ngono hukumbana hatari nyingi sana, na kuathirika kwa njia nyingi.

Akirejelea ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa ngono katika maeneo ya vita, Bi Bangura amepaza sauti ya kusimama bega kwa bega na wanawake wanaokumbana na uhalifu huu kote duniani ili kuutokomeza. Bi Bangura amesema hapawezi kuwepo mfumo wa usalama wa kuaminika ikiwa mfumo huo hauzingatii usalama wa wanawake.

“Ni muhimu tuendelee kutimiza wajibu wetu kwa manusura wa ukatili huu. Wapate msaada wanaohitaji, ushauri nasaha na msaada wa kisheria wanaohitaji ili kujenga tena maisha yao. Wakati huo huo, wanaotenda uhalifu huo ni lazima waelewe kuwa hawawezi kuwa na mahali pa kujificha, kusamehewa au kupata hifadhi salama. Kwa kufanya hivyo, tutaanza kuwahamishia wao unyanyapaa unaombatana na uhalifu huu kutoka kwa wahanga.”