UNAMID yataka misaada ya kibinadamu kwa raia huko Labado

17 Aprili 2013

Na sasa nchini Sudan ambako, baada ya vikosi vya Sudan Armed Forces kuutwaa mji wa mji wa Labado huko Darfur Mashariki, raia wanahitaji misaada ya kibinadamu kama anavyosimulia Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Kaneiya)

Baada ya mji huo wa Labado kutwaliwa jana kufuatia makali yaliyozuka kwenye eneo hilo yaliyosababisha vifo vya raia wanne na wengine sita kujeruhiwa, ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID, unatoa wito kwa pande husika kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia maelfu ya raia waliokuwa wamekimbia mapigano hayo mapya.

Inaelezewa kuwa mapema vikosi vya jeshi la Sudan viliendesha operesheni ya kulidhibiti eneo hilo asubuhi ya April 16 ambapo majeruhi wanatibiwa katika hospitali inayosimamiwa na UNAMID, karibu na mji huo wa Labado.

Aicha El Basr ni msemaji wa UNAMID.

(SAUTI YA AICHA)

"Mapigano yalikoma jana, na sasa tunaangalia misaada ya kibinadamu zaidi ambapo raia wamejikusanya katika ofisi za UNAMID huko Labado na Muhajeria na hadi sasa hawajapata misaada ya kibinadamu wanayohitaji. Hapo jana mratibu mkazi wa misaada ya kibiadamu ametaka pande zote hususan serikali kuruhusu misafara yenye misaada ya kibinadamu kufika kwenye miji hiyo na kutoa misaada inayotakiwa.”