Suluhu ya migogoro barani Afrika kumulikwa ndani ya Baraza Kuu la UM: Jeremic

16 Aprili 2013

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Vuk Jeremić amezungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani na kutangaza kuwa suala la usuluhishi wa migogoro barani Afrika kwa njia ya amani litamulikwa wakati wa mjadala wa wazi wa barazahilobaadaye mwezi huu. Bwana Jeremić amesema mfumo huo wa kuwa na mada maalum umekuwa wa mafanikio ambapo washiriki wanakuwa na fursa ya kujadili jambo kwa kina na kwamba mjadala kuhusu Afrika utakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU ambao kwa sasa unaitwa Umoja wa Afrika.

 (SAUTI YA VUK)

 “Huu utakuwa ni mjadala wa kwanza wa mada kuhusu Afrika, unafanyika wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika, viongozi kadhaa wa ngazi za juu wakiwemo Marais, mawaziri kutoka Afrika na nje ya Afrika watashiriki, na tunatarajia kuwa mjadala huu utaibuka na azimio kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa nchi huru za Afrika ambao kwa sasa ni Umoja wa Afrika.”

 Halikadhalika Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema mwezi Mei baraza litakuwa na mjadala wa wazi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, nishati inayojali mazingira na matumizi endelevu ya maji.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter