Mkutano wa pande tatu kuhusu UNAMID waangazia usalama Darfur

16 Aprili 2013

Hofu kuhusu ongezeko la visa vya kutokuwepo usalama na uwezo wa walinda amani wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa, Darfur (UNAMID) kuyafikia maeneo yaloathiriwa zaidi na mzozo yamefanywa masuala ya kipaumbele katika majadiliano ya kikao cha 15 cha mkutano wa mfumo wa pande tatu wa kuratibu shughuli za UNAMID.

Kikao hicho kimefanyika mnamo Jumatatu Aprili 15 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mfumo huo wa pande tatu unajumuisha serikali ya Sudan, Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa, na unalenga kusuluhisha matatizo na changamoto zinazohusiana na uwepo na operesheni za vikosi vya UNAMID.

Wakati wa mkutano huo, Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa zimeelezea wasiwasi kuhusu kuongezeka ripoti za mapigano ya silaha na ghasia za kikabila katika eneo la Darfur.

Huku ikizingatiwa kuwa ni wajibu wa serikali ya Sudan kuwalinda raia, ujumbe wa UNAMID umesema kuwa kuchelewesha kuwaruhusu walinda amani kuyafikia maeneo yenye mizozo kunaathiri vibaya na kudunisha utendaji kazi wa ujumbe huo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter