Mashirika ya Umoja wa Mataifa yapazia sauti watu wa Syria wasaidiwe

15 Aprili 2013

Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, leo kwa pamoja wamezipazia sauti pande zote katika mzozo wa Syria na serikali zenye ushawishi zifanye kila ziwezalo kuwaokoa watu wa Syria kutokana na watu wa Syria na ukanda mzima kutokana na baa la vita.

Wakuu hao, Valerie Amos wa OCHA, Ertharin Cousin wa WFP, Antonio Guterres wa UNHCR, Anthony Lake wa UNICEF na Margaret Chan wa WHO, wamesema ingawa ufadhili wa misaada bado unahitajika, ombi lao leo linahusu kitu kilicho muhimu hata zaidi kuliko fedha. Wamesema sasa ndio wakati wa kuchukua hatua za kukomesha mateso ya watu wa Syria.

Wameongeza kuwa mahitaji ya kibinadamu yanaendelea kuongezeka, huku uwezo wao kuwatimizia wanaoyahitaji ukiwa mdogo kutokana na sababu za kiusalama na uhaba wa ufadhili.

Wametoa wito kwa viongozi wa kisiasa wanaohusika na mzozo wa Syria kutimiza wajibu wao kwa watu wa Syria na ukanda mzima, na kusisitizia suluhisho la kisiasa kwa mzozo huo kabla  mamia ya maelfu ya watu zaidi kupoteza makazi na maisha yao.