Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lijikite katika kuzuia na si kutatua mizozo: Rwanda

Baraza la Usalama lijikite katika kuzuia na si kutatua mizozo: Rwanda

Baraza La usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala kuhusu jinsi ya kuzuia migogoro barani Afrika ambapo mwenyekiti wa mjadala huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda kama anavyo ripoti Joshua Mmali.

(SAUTI YA JOSHUA)

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao maalum kujadili suala la amani na usalama barani Afrika, na jinsi ya kuzuia mizozo hiyo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, amesema anataraji kuwa kupitia mjadala huo, Baraza la Usalama litaanza kuachana na desturi ya kudhibiti mizozo na badala yake kuanza kuzuia mizozo hiyo.

Bara la Afrika huchukua aslimia 68 ya ajenda ya Baraza la Usalama.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ingawa kikao cha leo kinaangazia bara la Afrika, kuna mafunzo ya ujumla katika kuzuia mizozo yanayoweza kuigwa na kutumika kote duniani.

Kwa mujibu wa Bwana Ban, mizozo hutokana na uongozi mbaya, ukiukaji wa haki za binadamu, na manung’uniko yatokanayo ukosefu wa usawa katika ugawaji wa rasilmali, utajiri na uongozi.

(SAUTI YA BAN)

“ Ili kuzuia mizozo, ni lazima tuimarishe demokrasia, tujenge taasisi thabiti za kitaifa zinazowajibika, tuhakikishe uwazi, tuendeleze uongozi wa kisheria, na kuhakisha tunaweka udihibiti tosha wa kidemokrasia dhidi ya vikosi vya kijeshi.”

Bwana Ban amesema katika ripoti yake kuhusu chanzo cha mizozo barani Afrika, ataangazia uongozi wa mzuri.