Uhifadhi wa rasilimali za aina za mazao ni muhimu kwa maisha ya binadamu

15 Aprili 2013

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kilimo na chakula duniani, FAO Dan Gustafson amewaeleza wajumbe wa tume ya uhifadhi wa aina mbali mbali za mazao duniani na kusema kadri idadi ya watu inavyoongezeka duniani na mahitaji ya lishe bora na ya kutosha inavyoongezeka ni lazima kuhifadhi rasilimali hizo kwa maisha ya binadamu.

(Taarifa ya Kaneiya)

Tume hiyo ya wajumbe kutoka nchi mbali mbali inakutana mjini Roma Italia ambapo Bwana Gustafson anasema usalama wa chakula ni changamoto kubwa hasa wakati huu ulimwengu unapokabiliwa na mabadiliko ya tabia katika nchi na ongezeko la idadi ya watu.

Amesema zaidi ya aina Elfu Saba za mimea imekusanywa na kupandwa tangu binadamu awe na ujuzi huo maelfu ya miaka iliyopita ilhali kuna zaidi ya aina Elfu Thelathini za mimea duniani inayofaa kwa chakula.

Amesema rasilimali za jeni za vyakula na kilimo zina umuhimu mkubwa katika uhakika wa chakula na huduma za kimazingira.

Halikadhalika zinawezesha mazao, mifugo na viumbe vya bahari kustahimili mabadiliko ya tabia nchi.

Inakisiwa kuwa mabadiliko ya hali ya hewa huenda yakapunguza mazao ya kilimo na mapato katika nchi nyingi ambazo tayari zinashuhudia uhaba wa chakula.