Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu ana fursa ya kuchochea kufikiwa kwa malengo ya Milenia: Ban

Kila mtu ana fursa ya kuchochea kufikiwa kwa malengo ya Milenia: Ban

Kampeni ya kuchochea utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia iliyoanza mapema wiki hii kwa kuhesabu siku Elfu moja zilizobakia kabla ya ukomo mwaka 2015, imetiwa shime hii leo hapa New York, Marekani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alipozungumza na wawakilishi wa nchi wanachama na wafanyakazi wa Umoja huo.

Bwana Ban amesema kila mtu, awe mwakilishi wa nchi wanachama au mfanyakazi ana nafasi yake ya kufanikisha malengo manane ya milenia ambayo kwa ujumla wake yanataka kutokomezwa kwa umaskini duniani. Amesema jitihada za serikali, taasisi za kiraia na wadau mbali mbali duniani zimewezesha kupatikana kwa mafanikio lakini bado kuna maeneo duniani yaliyo katika lindi la umaskini, ukosefu wa usawa na maji safi na salama.

(SAUTI YA BAN)

"Sasa ndio wakati wa kuongeza kasi ya MDGs. Sasa tumesalisha chini ya siku 1000 kuziba mapengo na kuongeza kasi ya hatua zetu. Hiyo inamaanisha kuongeza kasi ya kupanua ufanisi wetu, kuwainua wanawake na wasichana, kutimiza ahadi za kifedha, na kuchagiza watu tokea serikalini hadi mashinani. Mawazo na ari ya vijana ni muhimu has asana."

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa tangu nchi wanachama zipitishe malengo hayo mwaka 2000, umaskini uliokithiri umepungua kwa asilimia hamsini duniani na watu Bilioni Mbili wanapata maji safi na salama. Halikadhalika vifo vya wajawazito na watoto wachanga vimepungua na kwamba dunia bado inaendelea kukabiliana na magonjwa hatari kama vile Malaria, Kifua Kikuu na Ukimwi.