Ban akutana na Obama, masuala ya Syria, DPRK yapaziwa sauti zaidi

11 Aprili 2013

Katika Ikulu ya Washington DC hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekuwa na mazungumzo na Rais Barack Obama yaliyojikita juu ya Syria, Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK na mchango wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.

Kuhusu Syria Bwana Ban amesema amemsihi Rais Obama kudhihirisha uongozi katika kushirikiana na wadau muhimu ndani ya baraza la usalama na yeye kama Katibu Mkuu ataendelea kushirikiana na mjumbe maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na nchi za kiarabu.

Katibu Mkuu akatumia fursa hiyo kuisihi tena Syria kukubali timu ya uchunguzi ambayo aliiunda kufuatia ombi la nchi hiyo kukagua iwapo kuna matumizi ya silaha za kemikali.

(SAUTI YA BAN)

Rais Obama akatoa msimamo wake kuhusu suala la Syria.

(SAUTI YA OBAMA)

Kuhusu DPRK, viongozi hao wawili wameelezea kuguswa na sintofahamu iliyopo wakati huu katika rasi ya Korea kutokana na tishio la DPRK la kutaka kufanya jaribio la silaha ambapo Obama amesema nchi hiyo inapaswa kuacha mwelekeo wake wa kujenga hofu kwenye eneo hilo na badala yake izingatie maazimio ya Umoja wa mataifa wakati jumuia ya kimataifa ikiendelea kutatua masuala ambayo hayajapatiwa ufumbuzi.