UNHCR yapanua fursa ya elimu ya juu kwa wakimbizi

11 Aprili 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwa kushirkiana na shirika la huduma za wakimbizi la Jesuits, JRS linapanua wigo wa fursa ya elimu ya juu kwa wakimbizi na watu wengine waliofurushwa makwao kuweza kupata elimu  ya juu.

Elimu hiyo itakayotolewa kwa njia ya mtandao na madarasani inafuatia makubaliano kati ya pande mbili hizo ambapo fursa zinaongezwa kwa elimu mtandao huko Kenya, Malawi na Jordan na tayari pia kupanua mafunzo zaidi nchini Chad na mataifa mengine ambako UNHCR na JRS yanahudumu.

Mkurugenzi wa hifadhi ya kimataifa wa UNHCR, Volker Türk amekaribisha mpango huo na kusema hakikisho la kupata elimu ni haki ya msingi na kipaumbele kwa shirika katika operesheni zao zote.

Peter Balleis  ambaye ni Mkurugenzi wa JRS amesema wameshuhudia vile ambavyo elimu inawabadili wakimbizi na watu wanaofurushwa  makwao kuwa wasomi na hatimaye kuongoza nchi zao.

Halikadhalika amesema katika mazingira ya mizozo, elimu inaweza kuwapatia wakimbizi jibu la kiu ya kujenga upya jamii zao.

Mamia ya wakimbizi huko Jordan, Kenya na Malawi  tayari wamejiandikisha kwenye elimu mtandao katika Chuo Kikuu cha Regis hukoDenver,Colorado na vyuo vikuu vya taasisi ya Jesuits.

Mwaka jana UNHCR ilianzisha mkakati wa miaka mitano wenye lengo la kuongeza fursa za elimu kwa wakimbizi.