Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna mpango mpya wa kutokomeza kichomi na kuhara kwa watoto:WHO /UNICEF

Kuna mpango mpya wa kutokomeza kichomi na kuhara kwa watoto:WHO /UNICEF

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yamezindua mpango mpya wa kutokomeza vifo vya watoto vitokanavyo na kuhara na nimonia au kichomi katika muongo mmoja ujao. Flora Nducha ameandaa taarifa hii

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Mpango huo wa pamoja wa kuzuia na kudhibiti nimonia na kuhara wa shirika la afya WHO na lile la kuhudumia watoto UNICEF unatoa wito wa juhudi za pamoja za kukinga na kutibu maradhi hayo mawili.

WHO inasema mpango huo una lengo la kuokoa maisha ya watoto takriban milioni 2 wenye umri wa chini ya miaka mitano kila mwaka, hasa kwa kuongeza upatikanaji wa madawa muhimu , chanjo, lishe na mazingira safi.

Dr Elizabeth Mason wa WHO anasema nchi kama Bangladesh, Cambodia, Ethiopia, Malawi, Pakistan na Tanzania tayari wanafaidika na mpango huo

(SAUTI YA DR ELIZABETH MASON)

“Kupata matibabu rahisi kwa watoto wote ni muhimu saana . Hatuzungumzii toba za gharama, tunazungumzia kama oral rehydration salts ambayo chini ya sent kadhaa kwa pakiti, tembe za zinc na antibiotics ambazo nazo ni sent kadhaa. Tukijumuisha haya tuna mtazamo ambao ni wa kulinda, kuzuia na kutibu na kwa kuzingatia mambo haya matatu tunaamini malengo yaliyowekwa na mpango huu yanaweza kufikiwa. Na kwa mtazamo huo tunasema kwamba vifo vya nimonia kwa watoto wa chini ya miaka mitano inatakiwa kuwa chini ya vifo vitatu kati ya watoto 1000 na vya kuhara chini ya kifo kimoja kati ya vifo 1000”

WHO inasema ingawa kuhara na nimonia ni maradhi yynayozuilika , watoto wapatao milioni 6.9 wanakufa kila mwaka kutokana na maradhi hayo na hasa katika nchi zinazoendelea.