Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwepo wa mamia ya makundi madogo barani Afrika hatarini

Uwepo wa mamia ya makundi madogo barani Afrika hatarini

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya makundi madogo Rita Izsák ameonya kuwa mamia ya makundi ya aina hiyo barani Afrika yanatishiwa uwepo wao na hivyo serikali husika pamoja na jumuiya ya kimataifa zichukue hatua za dharura.

Ameibua hoja hiyo kwenye mkutano wa 53 wa Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Afrika huko Banjul, Gambia ambapo amesema ni muhimu kwa tume hiyo kuhakikisha pamoja na kwamba mara nyingi makabila madogo na makundi madogo katika kila nchi yanapatiwa kipaumbele, ni vyema kutosahau lahaja na dini ndogo ambazo nazo pia zinaimarisha utambulisho wa nchi husika.

Amesema kusimamia haki za makundi madogo ni njia muhimu ya kuzuia mvutano na pia ni msingi wa utawala bora.

Amesema ni jambo jema kuwa Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limetoa mapendekezo 70 kwa mataifa 30 ya Afrika juu ya masuala ya makabila na jamii ndogo, lakini changamoto ni nani atasaidia nchi hizo kutekeleza mambo hayo na nani ataziwajibisha iwapo zitakwenda kinyume.