Mateso yaghubika wafanyakazi wahamiaji Mashariki yaKati: ILO

10 Aprili 2013

Shirika la kazi duniani, ILO limetoa ripoti yake inayoonyesha madhila yanayowakumba wafanyakazi wahamiaji huko Mashariki ya Kati. Ripoti hiyo inasema kuwa zaidi ya wafanyakazi Laki Sita hutumikishwa katika kazi mbali mbali na ukatili wa kingono baada ya kunasa kwenye mtego wa kulaghaiwa. ILO inasema kuwa ijapokuwa ukanda huo una idadi kubwa ya wafanyakazi wahamiaji, bado sheria za kazi haziko makini kulinda maslahiyao. Mathalani wafanyakazi hao pindi wanapotaka kusitisha mkataba wa ajira au kubadilisha mwajiri hutishiwa kuwekwa kizuizini au kurejeshwa makwao. Helene Harrof-Tavel kutoka ILO anasema kutokuwepo kwa uhuru wa kutangamana katika nchi nyingi za kiarabu kunakwamisha harakati za wafanyakazi kupaza sauti zao.

 (SAUTI YA HELENE)

 “Watu wanaosafirisihwa kwenda Mashariki ya Kati si kwamba wanatekwa. Hawa ni wafanyakazi wahamiaji walio na ujuzi mdogo lakini wanatafuta kazi yenye staha. Wanakuwa wameahidiwa ajira Fulani au mazingira Fulani ya maisha, lakini pindi wanapofika huko wanakuta ndivyo sivyo, wamelaghaiwa. Wanakuwa wamenasa kwenye mtego unaowalazimu kutumikishwa kwenye ajira na hawawezi kuondoka. Mathalani tuangalie ajira za majumbani, kuna nchi moja tu ambayo imechukua hatua na kujumuisha ajira hiyo kwenye sheria zake, na nchi hiyo ni Jordan. Nyingine zote zimeandaa rasimu za sheria ambazo zimeibua mjadala. Lakini kuna tatizo kubwa kwenye sheria za ajira za majumbani na pia inajumuisha wafanyakzi wa sekta ya kilimo na kadhalika.”

 Ripoti hiyo ya ILO inapendekeza wizara za ajira huko Mashariki ya Kati zipatiwe uwezo wa kusimamia mchakato mzima wa ajira za wahamiaji, kushughulikia madaiyaona waajiri pamoja na kuthibtisha madai ya mateso na kuchukua hatua stahili.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter