Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamlaka za makundi ya Seleka bado yanawaingiza watoto katika jeshi: Vogt

Mamlaka za makundi ya Seleka bado yanawaingiza watoto katika jeshi: Vogt

Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Margaret Vogt, amesema kuwa uongozi wa kundi la Seleka lililonyakuwa mamlaka katika Jamhuri ya Afrika ya kati hauna utaratibu wa kisheria, na kuna ripoti za kundi hilo kuwashurutisha watoto kuingia katika jeshi.

Baada ya kulihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Bi Vogt amewaambia waandishi wa habari mjini New York kwa njia ya simu kuwa kinachosikitisha hata zaidi ni kwamba baadhi ya watoto waliokombolewa kutoka jeshi na Umoja wa Mataifa na kuunganishwa tena na familia zao, wameingizwa tena na makundi ya silaha.

Bi Vogt amesema hali ya kibinadamu bado ni mbaya sana, na kwamba wanaohitaji msaada hawawezi kufikiwa hasa kwa sababu za kiusalama, na uporaji wa maghala ya bidhaa za misaada

(SAUTI YA BI VOGT)

“Maghala yetu mengi ya kidinadamu yameporwa, wakati idadi ya wanaohitaji msaaada ikipanda, kwani takriban kila mwananchi anahitaji msaada wa aina moja au nyingine. Hali ya haki za binadamu pia imezorota sana, na visa vya uhalifu, ukiwemo ukatili wa ngono dhidi ya wanawake ambao uliripotiwa mikoani awali, lakini sasa pia jijini Bangui, ni suala la kutia wasiwasi. Haya ni mambo ambayo jamii ya kimataifa ni lazima itafute njia za kukabiliana nayo.”

Bi Vogt amesema, wakati jamii ya kimataifa inapojaribu kufanya juhudi za kurekebisha mfumo wa kisiasa na kuweka mfumo utakaoliweka taifa hilo kwenye mkondo taratibu, ni lazima pia suala la usalama lizingatiwe sana, kwani bila hilo, hakuwezi kuwepo suluhu la kudumu.