Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahabusu ya Guantanamo ifungwe:Pillay

Mahabusu ya Guantanamo ifungwe:Pillay

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa Navi Pillay Ijumaa amevitaka vitengo vyote vya serikali ya Marekani kufanyakazi pamoja ili kufunga kituo cha mahabusu cha Guantanamo akisema kuendelea kuwashililia mahabusu bila hukumu ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Amesema amesikitishwa na kitendo cha serikali ya Marekani kutoweza kufunga kituo cha Guantanamo Bay licha ya kurejea kuahidi mara kadhaa kufanya hivyo.

Inadaiwa kwamba karibu nusu ya mahabusu 166 ambao bado wanashikiliwa kwenye mahabusu hiyo wameshaidhinishwa kuhamishiwa ama katika nchi zao au nchi nyingine ambako itakuwa makao yao, lakini amesema bado wanashikiliwa Guantanamo Bay hadi sasa huku wengine wakiwa wamekaa kituoni hapo kwa zaidi ya muongo mmoja na wengine kutojua mustakhbali wao. Pillay amesisitiza kwamba hatua hii inazusha hofu na maswali mengi chini ya sheria za kimataifa, na inatia dosari msimamo wa Marekani wa kudai kwamba inathamini na kutimiza haki za binadamu na kudhoofisha uhalali wake wa kushughulikia masuala ya ukiukaji wa haki za binadamu kwengineko.

Bi Pillay amekumbusha kwamba miaka mine iliyopita alikaribisha tangazo la Rais Obama baada ya kuapishwa kwamba anatoa kipaumbele katika suala la kufunga mahabusu ya Guantanamo na kwa kuzingatia haki za msingi za mahabusu na anamtaka kutekeleza ahadi yake.