UNICEF kushirikiana na Mexico kuwasaidia maskini

4 Aprili 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na watoto UNICEF limezindua mpango maalumu nchini Mexico wenye shabaha ya kuzikwamua jamii maskini ikiwemo watoto.

Mpango huo ambao umezinduliwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya UNICEF na serikali ya Mexico unatazamiwa kuleta hali njema kwa mamilioni ya familia ambayo yanaandamwa na hali duni ya maisha.

Chini ya kichwa cha habari kisemacho utafiti juu ya hali ya umaskini kwa watoto na haki za kijamii kwa Mexico, mpango huo unatazamia pia kuangalia miundo ya kisera na vipaumbele vya kiuchumi.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Mexico Isabel Crowley amesema kuwa pamoja na kushuhudia kipindi kizuri cha ukuaji wa uchumi, lakini ukweli wa mambo bado watu wameendelea kuwa maskini.