Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuhifadhi mazingira, hatuna sayari nyingine ya kukimbilia: Ban

Tuhifadhi mazingira, hatuna sayari nyingine ya kukimbilia: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumza katika  jumba la makumbusho ya Sayansi ya Bahari nchini Monaco na kupongeza vile ambavyo nchi hiyo iko mstari wa mbele kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Bwana Ban aliyeko ziarani barani Ulaya, amesema  sera thabiti zilizopitishwa na nchi hiyo kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya magari ya umeme zinadhihirisha jinsi ilivyojizatiti kuendeleza uchumi unaojali mazingira. Halikadhalika amesema taasisi ya Mwanamfalme Albert wa II wa Monaco inaheshimika dunia nzima kwa kazi yake ya kupigia debe uhifadhi wa baionuwai, maji na vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Bwana Ban amesema kwa hifadhi ya mazingira ni miongoni mwa malengo ya maendeleo ya milenia, na kila mtu ana jukumu la kutekeleza wajibu wake kwa kuwa uharibifu wa mazingira bado ni changamoto kubwa. Amesema nchi za visiwa vidogo kamaKiribatizina hofu ya hatma ya uwepo wao kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba dunia ni moja na iwapo hali itakuwa mbaya hakuna sayari nyingine ya kukimbilia.