Kamishina mkuu wa UNHCR akaribisha muafaka mpya wa biashara ya silaha

3 Aprili 2013

Kamishina Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi Antonio Guterres leo amepongeza hatua ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa ya kuidhinisha mkataba wa kimataifa wa biashara ya silaha hapo Jumanne.

Amesema wakimbizi wanafahamu gharama za vita zaidi ya mtu mwingine yoyote, kwani kwao na mamilioni ya wakimbizi wa ndani kupitishwa kwa mkataba huo kulikuwa kunahitajika saana. Na ameongeza jukumu linalosalia ni kwa wote kuhakikisha utekelezaji wake.

Duniani kote kuna takribani wakimbizi milioni 15 ongeza na wakimbizi wa ndani milioni 26, na kwa kiasi kikubwa sababu ni vita vya kutumia silaha.

UNHCR kwa muda mrefu imekuwa ikitaka kuwe na utaratibu wa kudhibiti biashara ya silaha kama njia mojawapo ya kupunguza athari zake kwa maisha ya binadamu, kusambaa kwa silaha hizo na matumizi mabaya.