Homa ya mafua ya ndege yagundulika China

1 Aprili 2013

Shirika la afya duniani, WHO limeripoti kupatikana kwa wagonjwa watatu wa homa ya mafua ya ndege aina ya H7N9 nchini China.

WHO imesema imepokea taarifa kutoka Tume ya afya na kupanga familia nchini humo ikieleza katika maabara za China kuthibitisha ugonjwa tarehe 29 mwezi uliopita ambapo wagonjwa wawili wanatoka jimbo la Shanghai na mmoja Anhui.

Ripoti hiyo imesema wagonjwa wawili wamefariki  dunia na kwamba wote waligundulika kuwa na uambukizo katika mfumo wa kupumua.Vipimo vya virusi aina ya Novel Corona havikupatikana katika uchunguzi huo.

Hata hivyo hakuna maambukizi mengine yaliyotajwa katika ripoti hiyo ambapo inaelezwa ya kwamba uchunguzi zaidi unaendelea juu ya chanzo cha ugonjwa na maambukizi huku serikali ya China ikitangaza kuimarisha uchunguzi kwa kuboresha maabara, pamoja na kuwanoa wataalamu wa afya.

Kufuatia kugundulika kwa wagonjwa hao katika majimbo ya Shanghai na Anhui nchini China Shirika la afya duniani WHO, limesema linafanya mawasiliano na mamalaka husika nchini China kuchunguza kwa kina tukio hilo.