Wawakilishi wa wakimbizi waliotekwa nyara waachiliwe:Al-Za’tari

27 Machi 2013

Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Ali Al-Za’tari, ameelezea wasiwasi wake kuhusu taarifa za kutekwa nyara kwa wawakilishi wa wakimbizi wa ndani waliokuwa safarini kutoka Zalingei, Darfur Kati kwenda Nyala, Darfur Kusini kuhudhuria mkutano kuhusu wakimbizi wa ndani.

Al-Za’tari amesema msafara huo ulikuwa chini ya kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur, UNAMID.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa utekaji nyara huo umefanywa na wafuasi wa kikundi cha waasi cha Sudan Liberation cha Abdul Wahid Nur.

Al-Za’tari ametaka kuachiliwa mara moja kwa wawakilishi hao na kuelezea matumaini yake kuwa serikali ya Sudan na UNAMID watahakikisha wanarejea salama.