Baraza la Usalama lalaani Seleka, launga mkono hatua ya AU

26 Machi 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshutumu kitendo cha waasi wa kundi la Seleka huko Jamhuri ya Afrika ya Kati kupindua serikali na kusababisha majanga ikiwemo vifo na majeruhi kwa askari wa Afrika ya Kusini waliokuwemo nchini humo kulinda amani.

Kauli hiyo imetolewa baada ya kupokea taarifa ya hali halisi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kutoka kwa Naibu Msimamizi Mkuu wa masuala ya siasa ndani ya Umoja wa Mataifa  Tayé-Brook Zerihoun.

Taarifa ya baraza hilo imekariri wajumbe pia wakitambua uamuzi wa tarehe 25 mwezi huu wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika wa kusitisha ushiriki wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenye shughuli zote za Umoja huo pamoja na uamuzi dhidi ya viongozi wa kundi la Seleka ambao wamekiuka makubaliano ya Libreville na kusababisha uvunjivu wa amani na utulivu nchini humo.

Halikadhalika wametaka pande zote kujizuia kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani ikiwemo ukiukaji wa haki za kiraia na kuruhusu watoa misaada kufika maeneo yote bila vikwazo.

Wajumbe wa Barazahilo la usalama pamoja na kutaka wavunja sheria wote wawajibishwe, wamesisitiza nafasi muhimu ya Jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika ya Kati katika kuwezesha utekelezaji wa makubaliano yaLibreville kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud