Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa FAO asifu mwenendo wa uzalishaji chakula mdogomdogo vijijini

Mkuu wa FAO asifu mwenendo wa uzalishaji chakula mdogomdogo vijijini

Wakulima wadogowadogo, uzalishaji na ununuzi wa nyumbani pamoja na kuibua tena ukuzaji wa mimea ya kijadi kunaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza njaa, amesema leo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, wakati akiwahutubia wahadhiri na wanafunzi wa Chuo cha Sayansi ya Chakula nchini Italia.

Bwana da Silva ameelezea kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa ushirikiano baina ya FAO na chuo hicho katika kutimiza malengo ya kuwa na dunia isiyo na njaa na ambayo ni endelevu.

Amesema msisimko wa upandaji wa miaka ya 1960 ulikuwa umeongeza uwepo wa chakula kwa kila mtu kwa zaidi ya asilimia 40, lakini gharama yake ilikuwa ni kupoteza aina nyingi za mimea ya chakula kwa sababu ya kuangazia mimea michache tu, na athari kubwa kwa mazingira kutokana na matumizi ya kemikali za kilimo.

Amesema lakini sasa kuna ongezeko la mwenendo wa kuzalisha na kuuza vyakula vya kijadi, kuendeleza miundo mbinu vijijini na kuwasaidia wakulima wadogowadogo, na hivi vyote vinachangia kulinda mazingira na kuendeleza uchumi wa maeneo ya vijijini ambayo huathiriwa zaidi na njaa. Mifano ya vyakula vya kijadi alivyotaja ni mihogo barani Afrika na Amerika ya Kusini.