Ban ataka utulivu Jamhuri ya Afrika ya Kati

25 Machi 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani kile alichokiita kuchukua madaraka kwa njia isiyo ya kikatiba kulikofanywa na waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.  Bwana Ban amesema amesikitishwa na taarifa za ukiukwaji wa haki za binadamu, na kusisitiza juu ya kuheshimiwa kwa makubaliano ya amani ya Libreville ambayo amesema kuwa ndiyo yatayotoa suluhu ya kudumu.  George Njogopa na taarifa zaidi

(SAUTI YA GEORGE)

Katika taarifa yake, ametoa wito wa kurudishwa kwa utawala wa katiba haraka iwezekanavyo na kueleza kile alichoeleza ni masikitiko yake kutokana na taarifa za ukiukwaji wa haki za binadamu.  Ametaka wahusika wa ukiukaji huo watawajibishwa. Tangazo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa limefuatia hatua ya waasi kuuteka mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika Kati, Bangui, na kumlazimisha Rais Francois Bozize kuikimbia nchi.  Kwa upande mwingine, Ban amesema kuwa Umoja wa Mataifa unachukua hatua zote za tahadhari ili kuwalinda watumishi wake walioko nchini humo. Ripoti za hivi karibuni zimeeleza kuwa kiongozi wa waasi, Michel Djotodia, ambaye amejitangaza kuwa rais ameahidi kuidumisha serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa kulingana na makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwezi Januari.  Katika hatua nyingine, amempigia simu rais wa Ufaransa François Hollande,kujadilia hali hiyo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.  Pamoja na suala hilo la Jamhuri ya Kati, pia viongozi hao wamekuwa na majadiliano kuhusiana na mkwamo wa Mali na mzozo unaendelea nchini Syria.